Love Poem: Nitaolewa Kesho
Jacqueline  Njama  Avatar
Written by: Jacqueline Njama

Nitaolewa Kesho

Wasema subira yavuta kheri,
Kamba iliyovuta kheri yakatika,
Yakatika na Uzito wa huba, uliojawa na mahaba,
Na safari ya mapenzi, iliyojaza sheheni,
Kwake nimetia Nanga, sihitaji kivuko,
Nasema hivi, Nitaolewa kesho.
Haba na haba hujaza kibaba,
Kibaba kilichosheheni mapenzi ya Dhati,
Moyo ukafurika, kwa pepo za mapenzi yake,
Sihitaji feni zenyu, kwake upepo napata,
Nasema hivi, Nitaolewa kesho.
Safari ndefu ya mapenzi, iliyojawa machafuko,
Chombo alishikilia usukani, captain wa mapenzi,
Zake huba haziyumbishwi, kwa nyangumi au papa,
Nasema hivi, Nitaolewa kesho.
Hayawi hayawini sasa, yamekuwa na kunenepa,
Yanini kukondeana, wakati twashibana,
Sifurukuti hafurukuti, mapenzi Ndiyo nguzo yetu,
Nasema hivi, Nitaolewa kesho.
Yalianza kama chemichemi, sasa yafurika kama bahari,
Ilikuwa ni bahati, kufurika kwake hivi,
MUNGU AKITUJALIA, Hii ya kesho tatimia,
NASEMA HIVI, NITAOLEWA KESHO